Mwangwi wa
vilio na simanzi kutoka kwa watu waliopoteza maisha baada ya meli kuzama kwenye
mkondo wa bahari wa Nungwi, Zanzibar uliambaa kwenye maji na kwenda kugota
kwenye ukuta wa chini ya bahari, mahali palipokuwa na maelfu ya makaburi
yalichongwa kwenye mwamba mgumu kuhitimisha safari ya wote waliopoteza maisha yao
kwenye ajali hiyo ya kihistoria.
Kwa binadamu wa kawaida, wenye macho yanayoweza
kutofautisha giza na mwanga pekee, hiyo ilikuwa ni ajali ya bahati mbaya kama
zilivyo ajali nyingine lakini kwa wale wenye uwezo wa kuona zaidi ya upeo wa kawaida wa binadamu (beyond normal vision),
haikuwa ajali ya bahati mbaya bali kitu kikubwa zaidi kilichopangwa na
kuratibiwa kwa umakini wa hali ya juu.
“Babu! Mbona
nasikia vilio vya watu wengi sana!
Kwani kuna nini?” kijana mdogo anayefundishwa imani za kishirikina, Kahungo alikuwa
akimuuliza babu yake.
“Hivyo ni vilio
vya roho zilizopokonywa miili yao
bila kujiaanda.“
“Unamaanisha nini
babu?”
“Ili binadamu
akamilike anapaswa kuwa na mwili na roho, vitu hivi vinapotengana, binadamu
hufa. Sasa hawa wametenganishwa miili na roho ghafla kwenye ajali bila hata kujiandaa
na ndiyo maana wanalia sana.”
“Sasa mbona
wanazikwa wakiwa hai? Kwa nini wengine wanalia sana wakati wengine hawalii? Na hawa
waliokuwa wanachimba makaburi huku chini ya bahari walikuwa wanatumia vifaa
gani?”
Hawazikwi
wakiwa hai. Zile unazoziona ndiyo roho, zinapambana kurudi kwenye miili yao inayoelea juu ya maji
lakini zinashindwa. Wanaolia sana ni wale ambao
kwenye maisha yao
walimsahau Mungu na wakazama dhambini! Wale unaowaona hawalii ni wale ambao
walikuwa wanafuata maagizo ya Mungu. Waliochimba makaburi haya ya Nungwi
walitumia kitu chepesi sana, walitumia maarifa
ya giza!”
“Maarifa ya giza? Lakini mbona hata
misalaba inayowekwa kwenye makaburi haya siyo kama
ile tuliyozoea kuiona kule duniani? Naona kama ni mifupa ya binadamu imefungwa
na kutengenezwa misalaba,“ Kahungo alizidi kumhoji babu yake kwani kila alichokuwa
anakiona kilikuwa kinamshangaza.
“Hizi ni
kanuni za nguvu za giza!
Mbona hushangai mimi na wewe kufika huku chini ya bahari bila ya kuwa
mitungi ya gesi wala nini na bado
tunapumua kama kawaida?”
“Mh! Kweli
dunia ina mambo. Halafu nilisikia kuna wazamiaji kutoka kusini mwa Afrika walishindwa
kufika huku, mbona sisi tumefika kirahisi na bado naona watu wengi tu
wakiendelea na shughuli za mazishi?”
“Hii dunia
mjukuu wangu tunafaidi sisi wenye nguvu za giza! Hakuna kinachotushinda na ndiyo maana
nataka nikuandae na wewe ufuate nyayo zangu, si unaona mimi nimeshakuwa mzee! Kuna
kazi sana mpaka kufikia huku tulipo, unabidi
uvuke ngazi nyingi sana.
Wengi hata ngazi ya kwanza hushindwa kuivuka.”
“Kwani hapa
tulipo panaitwaje babu?”
“Nungwi! Kuna
mkondo bahari wenye nguvu sana
hapa na kuna wakati maji huwa yanachemka. Kutokana na maajabu ya hapa ndiyo
maana wachawi waliamua kuweka kituo chao kikuu. Maji yanapishana kwa ngazi
kuanzia juu hadi chini.
“Unataka
kusema hiki ni kituo cha wachawi?”
“Eee! Wengi
watashangaa kwa sababu ya ajali iliyotokea, lakini ukweli ni kwamba Nungwi ipo
kwa miaka mingi iliyopita. Hii siyo ajali ya kwanza kutokea hapa. Mimi tangu
nikiwa mdogo nilikuwa nakuja hapa kuongeza nguvu za kichawi na nilikuwa
nikishuhudia ajali kubwa kuliko hata hii.”
Maelezo ya babu yake yalimshangaza mno
Kuhungo. Alizoea kusikia au kusoma hadithi za kutisha kwenye vitabu lakini sasa
alikuwa eneo la tukio akishuhudia mwenyewe kila kitu. Babu yake akazidi
kumfafanulia mambo.
“Siyo binadamu
wote unaowaona duniani wanaishi kihalali, wengi hawafuati maagizo na mafundisho
ya Mungu! Wanavunja amri zake kwa makusudi. Wanaabudu sanamu na kutukuza
dhambi! Hawaogopi kufa wala adhabu za kaburi! Watu kama hawa wakiingia kwenye
mitego ya nguvu za giza
hawaponi!
“Sisi
(wachawi) huwa tunasaidia kuwafikisha kwa urahisi kuzimu kwa kuwapitisha kwanza
kwenye malago ya wachawi ambapo hutumikishwa kwa kipindi fulani kisha kuachwa
waendelee na safari zao. Miongoni mwa njia za kuwasaidia wafike upesi kwenye
safari zao ni kuwazika chini ya bahari.
“Babu! Unataka
kusema makaburi chini ya bahari hayapo hapa Nungwi pekee?”
“Yapo sehemu
nyingine nyingi, lakini kwa miaka mingi hapa ndiyo kwenye makaburi maarufu na
mengi zaidi, ndiyo maana hata mkondo bahari wa hapa una nguvu kubwa na husababisha
ajali nyingi na kubwa kuliko sehemu nyingine.”
“Aaah! Mbona
unanichanganya! Kwani kilichoanza kuwepo hapa Nungwi ni makaburi ya chini ya
bahari au mkondo wenye nguvu unaosababisha ajali?”
Swali lile
lilimfanya yule mzee amkazie macho mjukuu wake huku akiwa ni kama
ambaye hakutegemea kulisikia kutoka kwake. Aliachia tabasamu hafifu kisha
akasema:
“Naona umekua
siku hizi mjukuu wangu kwani unauliza maswali ambayo hata mimi nilipokuwa na
umri kama wako sikuweza kuyafikiria. Kwa kuwa
una hamu ya maarifa juu ya ulimwengu usioonekana kwa macho ya kawaida, nitakufafanulia
kila kitu.”
“Cha kwanza
kuwepo ilikuwa ni kituo kikuu cha wachawi miaka mingi sana iliyopita. Kutokana na nguvu za giza zinazozalishwa chini ya bahari kila wachawi kutoka sehemu
mbalimbali wanapokutana, maji yalikuwa yakivurugika sana na kuchemka, ndiyo mkondo wa bahari ukaanza
kutokea taratibu kisha ukawa unazidi kuongezeka nguvu.
“Mkondo huo ulianza
kusababisha ajali nyingi kwa wasafiri wa majini na kupoteza maelfu ya roho za
watu, waliokuwa wanakufa wakawa wanaletwa kuzikwa huku chini, ndiyo yakatokea
makaburi haya ambayo yalizidi kuongezeka wingi kwa kadiri ajali zilivyokuwa
zinazidi kutokea.”
Baada ya kukaa
kule chini ya bahari kwa saa nyingi. Kahungo akishuhudia mauzamauza mengi ya
kichawi, alimuomba babu yake waondoke kwani moyo wake ulishindwa kuvumilia yale
aliyokuwa anayaona na kuyasikia. Wakashikana mikono na babu yake kisha
wakafanya ishara za kichawi, Kahungo akaambiwa afumbe macho kama
alivyofanya awali wakati wa kuja. Kufumba na kufumbua wakajikuta wako mchangani,
ufukweni mwa bahari.
naitaka yote hii hadisi ila sijui nifanyeje. maana kila niingia kuitafuta hua naipata kipandetu siipati kamili. nifanyeje mkuu nipe mbinu
ReplyDeleteTUTAKUTUMIA
ReplyDeleteNtaipataje naitaka yote mkuu
ReplyDeleteHongera Mkuu,ila Hata Mimi Naitaka Yote Sijuw Nifanyeje!
ReplyDeletenaitaka yote jaman naomba mwendelezo!!!!
ReplyDelete